Huzuni ikipitiliza humpelekea mtu
kukata tamaa na kutoona thamani ya maisha na hata kufikia hatua ya kunywa sumu
au kujiua wakati furaha ikizidi humfanya mtu akasahau majukumu mengine mazito
yaliyo mbele yake.
Matokeo ya
kidato cha nne yaliyotoka hivi karibuni yamewaacha wanafunzi na wazazi wengi
kwenye majonzi huku wengine wakiwa na furaha. Hii ni kutokana na idadi ya
wanafunzi waliomaliza kuwa na matokeo ya wastani katika mitihani yao.
Pamoja na hilo,
kubwa ni kuangalia namna bora ya kusonga mbele kwa wale ambao hawakufanya vema
wakijipanga upya kuangalia ni yepi ya kufanya ili kuweza kusonga mbele baada ya
jitihada zao zilizotangulia kutofanikiwa wakati wale waliofaulu vizuri wakiweka
mipango na mikakati madhubuti itakayowawezesha kuendelea zaidi.
Jambo la kwanza
analopaswa kulitambua mwanafunzi ni kukubali matokeo aliyoyapata. Kuukana
ukweli huu hakutakuwa na msaada kwake. Ni wazi zinaweza kuwapo kasoro za hapa
na pale katika masuala ya usahihishaji lakini mchango wake katika matokeo ya
jumla unaweza usiwe mkubwa sana.
Kwa muhtasari,
matokeo ya kidato cha nne unaweza kuyagawa katika makundi yaliyopangwa katika Muundo
wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Points Average ama GPA) ambayo ni
daraja la ‘A’ kundi la fauli Uliojipambanua (Distinction) litakuwa na alama
kati ya 3.6-5.0, ‘B’ Kundi la Kundi la ufaulu mzuri (Merit) litakuwa na alama
kati ya 2.6.3.5, ‘C’ kundi la ufaulu wa wastani (Credit) litakuwa na alama kati ya 1.6-2.5, ‘D’ Kundi
ufaulu hafifu (Pass) 0.3-1.5 na ‘F’ Kundi
la ufaulu usioridhisha (Fail) 0.0-0.2.
Aidha unaweza
kuyagawa katika makundi manne ya walio na sifa za kuendelea na kidato cha tano
na vyuo vya ufundi; wasio na sifa za kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya
ufundi lakini wana fursa za kuendelea na vyuo vingine; na waliofeli kabisa
amabo wanakosa sifa za kuendelea na masomo kwa vigezo vya ufaulu wa kidato cha
nne.
Kujiunga kidato
cha tano na vyuo vya ufundi
Awali ya yote
ifahamike kuwa wanafunzi wanaochaguliwa moja kwa moja kujiunga na kidato cha tano
au vyuo vya serikali ni wale wanaotoka shuleni (school candidates) na si watahiniwa
wa kujitegemea (private candidates).
Kadhalika
wanafunzi wanaochaguliwa moja kwa moja katika vyuo vya ufundi mfano Dar es
Salaam Institute of Technology (DIT), Arusha Institute of Technology (AIT) na
kama hivyo, huwa na sifa sawa na wale wanaochaguliwa kuijunga na kidato cha
tano katika michepuo ya sayansi. Idadi ya wanafunzi hawa huwa si kubwa sana.
Mwanafunzi
aliyefaulu kwa Distiction na Merits ana nafasi kubwa ya kuchaguliwa kuendelea
na masomo ya kidato cha tano au chuo cha ufundi katika shule na vyuo vya
serikali. Aidha hata waliopata Credit na Pass wana nafasi ya kuchaguliwa. Si
tukio la kawaida mwanafunzi aliyepata divisheni F kuchaguliwa kujiunga kidato
cha tano au chuo cha ufundi.
Mara nyingi
changamoto wanayokuwa nayo wanafunzi waliofaulu kwa viwango vya juu ni aina ya
michepuo na shule za kuendelea nazo. Ni jambo la kawaida kukuta kijana akifaulu
masomo mengi na kisha kusoma mchepuo ambao hana mapenzi nao sana. Hili
husababishwa na mazingira ya ujazaji fomu za michepuo ya kuendelea nayo baada
ya kuhitimu masomo. Hutokea kuwa mchepuo anaoupenda sana ana shaka ya kufanya
vizuri na hivyo kuchaguwa michepuo mingine. Ama kwa upande wa shule,
hutegemeana na nafasi, ufaulu wa wanafunzi na idadi ya wanafunzi walioomba
katika Shule husika.
Baadhi ya
wanafunzi wanapokosa michepuo au shule walizoomba huhangaika na kutumia muda
mwingi wakitaka kubadilisha. Uzoefu unaonyesha kwamba ni sehemu ndogo za sana
ya wanafunzi hao ambao hufanikiwa. Ushauri wetu ni kwamba endapo kijana
atachaguliwa katika shule asiyoipenda na hakuna sababu za kiafya za kumfanya
asiende katika shule hiyo pengine kutokana na hali ya hewa, au kachaguliwa
mchepuo asioupenda na familiya yake haina uwezo wa kumsomesha shule binafsi,
basi atulizane katika hicho alichopata na ajikite zaidi katika masomo kwani
anaweza pia kufanikiwa katika fursa hiyo aliyoipata.
Changamoto
nyingine ambayo huwakuta vijana wa kundi hili ni kuanza kusoma tuisheni za
masomo ya kidato cha tano kabla ya uchaguzi kufanyika. Utata wa jambo hili ni
kama tulioueleza hapo juu wa mwanafunzi kuchaguliwa mchepuo tofauti kabisa na
masomo anayosoma. Kwa mfano kuna kijana tunayemfahamu akisoma masomo ya mchepuo
wa Economic, Geography na Mathematics (EGM) lakini akachaguliwa mchepuo wa
History, Kiswahili na Language (HKL). Tofauti iliyoje! Katika hilo inashauriwa
kuwa kama mwanafunzi hana hakika ya kusoma katika shule binafsi, asianze masomo
hayo mpaka baada ya uchaguzi wa kidato cha tano kufanyika. Na ikibidi kujisomea
asome vitu vya jumla kama masomo ya lugha, kompyuta nk.
Kwa wale
waliokwisha amua au lazima wasome katika shule binafsi, ni muhimu kufanya
utafiti juu ya ubora wa shule hizo kitaaluma, maadili na stadi nyingine za
maisha. Aidha ni muhimu kufuatilia juu ya kiwango cha ada, muda wa kuchukuwa na
kurejesha fomu za maombi, tarehe ya usaili na ya kufungua shule. Hutokea
mwanafunzi akapoteza muda na hatimaye kuhangaika kutafuta shule wakati shule
nyingi zimeshasimamisha kupokea wanafunzi.
Kuna wanafunzi
waliopata Pass na Credit ambao hawatapata nafasi ya kujiunga na kidato cha
tano. Hata hivyo vijana waliopata Pass na sehemu ndogo ya waliopata Credit huwa
wanapata sifa na wanaweza kujiunga na kidato cha tano katika shule binafsi
endapo uwezo wa familiya unaruhusu. Hii ni kutokana na kanuni za Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambazo zinamruhusu mwanafunzi kuendelea na masomo ya
kidato cha tano endapo amefaulu katika kiwango cha angalau alama C kwa masomo
matatu au zaidi hata kama masomo aliyofaulu hayatengenezi mchepuo wowote mfano
Civics, Biology na English huku akiwa amepata alama D au chini yake katika
masomo mengine. Endapo familiya itamudu kumsomesha kidato cha tano kati shule
binfasi, ni vema kijana akapata ushauri wa wazazi, walimu na wazoefu wengine
juu ya mchepuo stahiki inayomfaa. Mara nyingi wanafunzi wa aina hii huwa
wanashindwa kutofautisha baina matashi ya nafsi na uwezo binafsi wa kimasomo.
Kwamba kijana tuliyemtaja hapo juu asome CBG au HGL ni suala linalohitaji
tafakuri pamoja na mhusika.
Kujiunga na
vyuo vya Ualimu
Kuna wanafunzi
waliopata Pass na hata Credit ambao hawatachaguliwa kujiunga na kidato cha tano
lakini watachaguliwa kujiunga na vyuo vya ngazi ya Diploma mfano vyuo vya
Ualimu. Kwa mujibu wa kanuni zilizopo sasa, kiwango cha ufaulu cha mwisho
kuchukuliwa ni Credit. Pamoja na kujaza nafasi za masomo ya Ualimu, mwanafunzi
atapaswa kuomba rasmi nafasi hizo kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi
au katika vyuo binafsi baada ya matokeo kutoka na nafasi kutangazwa rasmi.
Aidha kutokana na uchache wa nafasi katika vyuo huwa si wote walio na sifa
wanaoweza kuchaguliwa serikalini lakini nafasi ni nyingi sana katika vyuo
binafsi.
Kujiunga na
Vyuo Vingine
Wapo vijana
ambao licha ya kuwa na sifa za kuchaguliwa katika vyuo vya ualimu, huwa
hawachagui au hawaendi hata baada ya kuchaguliwa kwasababu zao binfasi. Kama
uwezo wa familia unaruhusu na mnaona kusoma ualimu si kipaumbele chenu haina
tatizo. Hata hivyo, ni vema kuangalia fursa zilizopo na uwezo wa familia kiuchumi.
kijana anapaswa kufahamu kufahamishwa kuwa si busara kwa familia yenye uwezo
duni wa kiuchumi, kama zilivyo familia nyingi za kitanzania, kumsomesha kijana
katika ngazi hii kwa gharama kubwa wakati kuna wengi wanahitaji kuendelezwa
kitaaluma katika familia.
Wale wote
waliokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha tano, vyuo vya ufundi, vyuo vya
kawaida au vyuo ualimu, fursa pekee waliyonayo ni kujiunga na vyuo vingine
vinavyotoa kozi mbalimbali kama, biashara, utawala, ufundi, nk. Vyuo kama
College of Business Education (CBE), Tanzania Institute of Accountancy (TIA),
Institute of Social Work (ISW), Institute of Information Technology (IIT) ni
mifano michache katika ya vyuo vingi vilivyopo. Changamoto kubwa katika vyuo
hivi ni uwezo wa kuzimudu gharama zake za mafunzo hayo.
Mwanafunzi
aliyefeli kabisa na kupata Sifuri (0), hana fursa yoyote katika zote
zilizotajwa hapo juu. Hata hivyo anakuwa amepata cheti cha kuhudhuria masomo
(leaving certificate) ambacho huwa na msaada fulani katika maisha kwa kuna
wakati huhitajika vijana waliomaliza kidato cha nne bila kujali ufaulu wake.
Pia kuna fursa
zinazohitaji vijana waliomaliza shule ya msingi ambazo bado zinaweza kutumiwa
na vijana hawa. Kwa mfano kuna fani mbalimbali zinazotolewa na vyuo vya VETA
kama ufundi, udereva, usafi,utunzaji bustani, upishi nk ambazo zinaweza
kutumiwa vema na vijana ambao hawakufaulu mitihani ya kidato cha nne.
Ni muhimu
kutaja hapa kwamba si waliofeli tuwanaoweza kuzitumia fursa za mafunzo ya VETA
bali hata wale waliopata divisheni Pass na hata Credit ambao ama hawakupata
fursa za kuchaguliwa kidato cha tano au familiya zao hazimudu kuwasomesha
katika shule au vyuo vya kujilipia.
Kurudia
Mitihani
Wanafunzi wengi
wanaofanya vibaya katika mitihani yao, jambo la haraka linalowajia vichwani ni
kurudia mitihani. Ndio maana siku hizi vituo vinavyotoa mafunzo kwa wanaorudia
mitihani vimekuwa vikiongezeka kila kukicha. Ni kwakuwa soko linakuwa na wateja
wameongezeka.
Pamoja na
kuunga mkono na kuheshimu juhudi za wanaotoa mafunzo hayo, tungependa
tutanabahishe kwamba ni ili kuepusha upotevu mwingi wa muda na pesa, ni vema
mwanafunzi akawa akijiandaa kurudia mitihani huku akijufunza ujuzi mwingine.
Uzoefu unaonyesha kuna wanafunzi wanaorudia mitihani na matokeo yao kuwa mabaya
kuliko ya mwaka uliotangulia. Aidha kuna wanafunzi waliorudia mitihani zaidi ya
mara moja na bado hawakufanikiwa kupata alama C au zaidi (credits) tatu
walizohitaji ili wajiunge na kidato cha tano.
Endapo
mwanafunzi atajiandaa kurudia mitihani huku anapata ujuzi mwingine mfano
udereva, ufundi,nk anakuwa katika nafasi nzuri ya ajira hata asipofaulu
mitihani yake anayorudia. Ni uzuri ulioje endapo atapata vyote - credits na
huku ana cheti cha ujuzi wake.
Jambo hili
linawezekana endapo kijana ataugawa vizuri muda wake chini ya muongozo wa
familia kwa mfano asubuhi akienda chuoni kupata ujuzi na jioni akienda tuisheni
kwa ajili ya kurudia mitihani. Aidha endapo mwanafunzi hatofanikiwa kupata
credits, anaweza kuanza kazi huku ajiandaa taratibu kurudia mitihani yake.
Wengi wamefanikiwa kwa utaratibu huu.
Kukata rufaa
juu ya matokeo
Wapo wanafunzi
ambao wanakuwa hawakuwa hawakuridhika na matokeo waliyopata wakiamini
hawakutendewa haki katika usahihishaji pengine kwa kuzingatia rekodi za matokeo
yao katika mitihani ya shuleni au kwa jinsi walivyofanya mitihani.
Kwamba
hatupingi jambo hili ndivyo pia tungependa kusisitiza kuwa wakati ukikusudia
hilo ni vema ukaendelea na mipango mingine ya kujiendeleza kama tulivyoitaja
hapo juu. Hii ni kwasababu ni wanafunzi wachache sana ambao matokeo yao
hubadilika baada ya mitihani yao kusahihishwa upya. Aidha unaweza kupoteza muda
mwingi ukisubiri hatma ya rufaa yako na kisha majibu kuja usivyotarajia.
Ufadhili wa
Masomo
Hutokea
wanafunzi waliopata nafasi za masomo katika shule binafsi au vyuo vinavyohitaji
kujilipia wakawa hawana uwezo wa kujisomesha na hivyo kuhangaika huku na kule
kutafuta ufadhili. Ukweli ni kuwa ni wachache sana ambao hufanikiwa. Hii ni
kutokana na kutokuwa na taasisi rasmi zinazotoa ufadhili katika viwango hivi ya
elimu nchini.
Pamoja na
kutokatishana na tamaa, ni vema mtu unapokuwa katika hali hiyo kutafuta
shughuli itakayokuwezesha kujenga nguvu za kiuchumi na kisha kuweka akiba kwa
ajili ya kujisomesha. Unaweza kuweka malengo ya kusoma huku ukifanya kazi.
Endapo shughuli zako hazikupi fursa ya kusoma huku ukifanya kazi, unaweza
kuahirisha kusoma hadi kipindi fulani baada ya kujiimarisha kiuchumi. Endapo
hilo litakuwa gumu kulitekeleza, familia iangalie uwezekano wa kuuza sehemu ya
rasilimali endapo inazo na ambazo hazitaithiri familia nzima endapo zitauzwa.
Tuhitimishe kwa
kusema, matokeo vyovyote yawavyo hayawezi kuwa ndio mwisho wa maisha. Siku zote
wanaofanikiwa ni wale wanaotazama mbele huku wakijifunza kwa yaliyowatokea.
Walofaulu washukuru huku wakijipanga; waliofanya vibaya wasubiri huku
wakijifuza. Tumia vizuri kila fursa unayoipata bila kujali udogo wake. Jifunze
kwa wengine, uliza, pata miongozo kwa waliokutangulia, na amini kuwa ipo siku
ufanikiwa. Washindi hawaachi, na wenye kuacha hawashindi.
KUVUNJIKA KWA
KOLEO SI MWISHO WA UHUNZI
Kwa Msaada
zaidi wa ushauri na namna bora ya kusoma tafadhali wasiliana nasi kwa namba 255
767 488856
au barua pepe marshk86@hotmail.com
Chanzo ni mbeyayetu
No comments:
Post a Comment