WAZIRI
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amewaomba
Watanzania kusubiri kwa hamu siku ya kutangaza nia ya kuwania urais kwa
tiketi ya CCM, katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Membe amesema,
amepanga kutangaza nia hiyo, Juni 6, mwaka huu, na kuwaomba wananchi
wamsikilize kwa makini siku hiyo kwakuwa ataeleza kwa kina nini anataka
kufanya nchi iweze kuondoka ilipo ikiwemo kuendelea kudumisha amani na
utulivu uliopo.
Waziri Membe ambaye hajatangaza rasmi nia yake ya
kuwania Urais, lakini ambaye ni miongoni mwa wanaotarajiwa kutikisa
katika kuwania kiti hicho, alitoa mwito huo jijini Dar es Salaam jana,
katika Tamasha la Qaswida lililofanyika kwenye viwanja vya Shule ya
Sekondari ya Benjamini Mkapa.
“Mkae tayari siku hiyo, naamini
uongozi mzuri wa nchi ni ule wa kudumisha amani na utulivu na ili nchi
iweze kusonga mbele, suala la uadlifu ni lazima kupewa kipaumbele kwa
viongozi alisema,” alisema Waziri Membe
"Ninawapongeza sana, kwa
kuamua kuwajenga vjana katika maadili ya dini, msingi huu ndio unaoweza
kuifanya Tanzanaia kuwa na viongozi walio bora kutokana na hofu ya
Mungu, maana mtu asiye mchamungu hawezi kukosa kuwa mla rushwa, fisadi
na mtumiaji mbaya wa madaraka" alisema Membe.
Membe alitumia
nafasi hiyo kuwatahadharisha kuwa makini katika kipindi hiki cha
uchaguzi mkuu, kuacha kuchagua viongozi ambao kwa nje, wanajinadi kuwa
wachamungu, lakini matendo yao hayaendani na maadili ya dini zao.
Alisema
moja ya dalili za viongozi wasiokuwa waadilifu kwa kutokuwa na
uchamungu huwa ni kusaka uongozi kwa kutumia fedha nyingi hivyo
amewasihi wasiwachague viongozi wa aina hiyo wanaosaka uongozi kwa kutoa
rushwa.
“Msikubali kuwa na viongozi ambao kwa nje, wanaojinadi
kuwa na dini kinyume na matendo yao, lazima mchague wenye hofu ya Mungu
jambo ambalo limekuwa likisisitizwa na dini zote. Uongozi wa heshima ni
ule unaochukia rushwa ambayo ni adui wa haki", alisema Membe.
Kuhusu
tamasha hilo, Waziri Membe alipongeza uwepo wake ambapo ni kuwalea
vijana katika maadili mema ya kumjua Mungu na kusema anajivunia Taasisi
za aina hiyo.
Tamasha hilo lililodhaminiwa na Kampuni ya Dira ya
Mtanzania chini ya Mkurugenzi wake Alex Msama, zaidi ya vikundi 50
vimeshiriki tukio hilo la aina yake.
Akizungumza katika Tamasha
hilo, Mkurugenzi wa Ulamaa Promotion Center ya jijini Dar es Salaam,
Jumanne Ligopora, alihimiza umuhimu wa kila mtu kuwa sehemu ya ulinzi wa
amani na utulivu.
Mwishoni mwa Tamasha hilo, Membe, alikabidhi
tuzo kwa watu mbalimbali na pia Membe mwenyewe kupewa tuzo kutokana na
kutambua mchango wake katika masuala ya kijamii.
No comments:
Post a Comment